Header Ads

ad

Breaking News

Moro United, Ruvu JKT sare

MORO United na Ruvu JKT, jana zilitoka sare ya mabao 2-2, katika mechi ya Ligi Kuu Bara iliyochezwa kwenye Uwanja wa Azam Chamazi, Dar es Salaam.

JKT Ruvu ilikuwa ya kwanza kulifikia lango la wapinzani wao, dakika ya sita, Hussein Bunu, alilifikia lango la Moro United, lakini alikutana na kizingiti cha kipa Lucheke Gaga aliokoa mchomo huo.

Moro United ililifikia lango la JKT Ruvu na kujipatia bao dakika ya 35, lililofungwa na Henry Ng'onye, kwa kuunganisha mpira wa krosi uliopigwa na Godfrey Wambura.

Dakika ya 67, Hussein Bunu aliisawazishia JKT Ruvu bao kwa kuunganisha kwa kichwa krosi iliyopigwa na Rajab Chau.

Moro United walipata bao la pili dakika ya 79, kupitia kwa Gaudence Mwaikimba, lakini Alhaji Zege aliisawazishia JKT Ruvu bao hilo dakika ya 81.

Kutoka Kagera, Mwandishi Wetu anaripoti kuwa, Oljoro JKT iliibuka na ushindi wa mabao 2-1, dhidi ya Kagera Sugar, mechi iliyopigwa Uwanja wa Kaitaba mjini Bukoba.

Bao la kwanza la Oljoro lilifungwa na Amir Omari dakika ya nne, baada ya kuwazidi ujanja mabeki wa Kagera Sugar na kuukwamisha mpira wavuni.

Oljoro JKT ilijipatia bao la pili dakika ya 25, kupitia kwa Omari, bao lililowachanganya wapinzani wao. Kagera Sugar ilipata bao dakika za mwisho za mchezo.

Kutoka Pwani, Omari Mngindo anaripoti kuwa, Ruvu Shooting imeibuka na ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya African Lyon, kwenye Uwanja wa Mlandizi mkoani Pwani.

Bao la kwanza la Ruvu lilifungwa dakika ya  28, kupitia kwa Kassim Linde na bao la pili la washindi lilipachikwa wavuni dakika ya 89, Abrahman Abrahman.

No comments