Header Ads

ad

Breaking News

Mustapha Hasanali azindua nembo ya Swahili Fashion Week


Maonesho ya nne ya mavazi ya Swahili fashion week,  yamezinduliwa Dar es Salaam jana na Mkurugenzi wa Baraza la Sanaa Taifa (BASATA), Gonche Matelego.

Akizundua nembo ya maonesho hayo,  Matelego amesema BASATA inahakikisha ubunifu unatunzwa kwa kuwa ni moja ya utamaduni wa watanzania unaotokana na sera ya ubunifu.

Amesema maonesho ya Swahili Fashion week ni moja ya maonesho yanayoenzi utamaduni wa mtanzania kwa kuwa maonesho hayo ya mavazi yamelenga zaidi kuonesha mavazi ya asili ya mtanzania.

Matelego alimpongeza mwandaaji na mwanzilishi wa maonesho hayo,  Mustapha Hasanali kwa kubuni kitu pekee kitakachowakumbusha watanzania asili ya mavazi yao kupitia maonesho hayo.

Pia, ametoa changamoto kwa Hasanali na wabunifu wote, kubuni vazi la Taifa ambalo hadi sasa,  Tanzania haina vazi maalum la Taifa kama zilivyo nchi nyingine.

Hasanali amesema mwaka huu yatashirikisha wabunifu 50 kutoka nchi nane za Afrika, ambapo yataadhimisha pia miaka 50 ya Uhuru, huku yakifanyika katika Mkoa wa Arusha.

Amesema jumla ya wabunifu 20 chipukizi watachuana katika maonesho hayo na kwamba, tayari mchakato wa kuwapata chipukizi hao, umeanza.

Amesema maonesho hayo yataanza Novemba 10 hadi 12, mwaka huu katika Makumbusho ya Taifa na yatafanyika sambamba na warsha kwa wabunifu, huku kukitolewa tuzo ya mbunifu bora wa Swahili fashion week.

Amesema wabunifu bora wawili watapata nafasi ya kushiriki maonesho ya wabunifu yatakayofanyika nchini Angola.

Maonesho hayo ambayo yalianza rasmi mwaka 2008, mwaka huu yamedhaminiwa na Southern Sun, Precisen Air, BASATA, Amarula, Redd's, Ultimate security, Image Masters, Vayle spring na 361 Degree.

No comments